Na.
James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam
Tarehe 13 Machi, 2021
Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Humprey Polepole (Mb)
amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kina jukumu la kuhakikisha kinaendelea
kujenga nidhamu na uadilifu kwa watumishi wa umma na viongozi katika Utumishi
wa Umma ili waweze kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.
Mhe. Polepole ametoa rai hiyo mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa anayoiongoza kutembelea makao makuu ya Chuo cha Utumishi wa Umma jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya chuo hicho chenye dhamana ya kutoa mafunzo kwa Watumishi wa Umma yanayowawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mhe. Polepole amesema, chuo hakina budi kuendelea kutoa mafunzo yenye tija ili kizazi kipya kilichoingia na kinachoendelea kuingia katika Utumishi wa Umma kiendelee kuishi katika mila, utamaduni, desturi na miiko ya Utumishi wa Umma.
Mhe. Polepole amefafanua kuwa, Utumishi wa Umma nchini umejengeka katika mila, utamaduni, na desturi, hivyo Chuo cha Utumishi wa Umma pekee ndio kina jukumu la msingi kuhakikisha kinatoa mafunzo ambayo yatajenga utamaduni utakaoimarisha nidhamu ya utendaji kazi, uadilifu na uzalendo kwa Watumishi wa Umma.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na
Serikali za Mitaa kuwa, suala la kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma kiutendaji
na nidhamu limepewa uzito unaostahili na ofisi yake kwa kuwataka waajiri wote
kuhakikisha wanatenga bajeti itakayowawezesha watumishi wao kupata mafunzo
yanayotolewa katika Chuo cha Utumishi wa Umma.
Aidha, Mhe. Ndejembi amewaomba wajumbe wa kamati hiyo kutumia mamlaka waliyonayo kushirikiana na Ofisi yake kuwahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Taasisi za Umma kutenga fedha zitakazowawezesha Watumishi wa Umma kupata mafunzo katika Chuo cha Utumishi wa Umma.
Mhe. Ndejembi ameiahidi kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ili kuboresha huduma zinazotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.
Chuo
cha Utumishi wa Umma Tanzania kilianzishwa kwa lengo la kutoa mafunzo katika
Nyanja za uongozi, menejimenti na utawala kwa ngazi za Cheti, Stashada na
Astashahada. Pia chuo kinafanya utafiti na kutoa ushauri wa kitaalam.
Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humprey Polepole (Mb) akiwahimiza
Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Kampasi ya Dar es Salaam
kutoa mafunzo yatakayowajengea Watumishi wa Umma nchini nidhamu ya Utendaji
kazi na uadilifu.
Baadhi
ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa na
watumishi wa TPSC wakisikiliza maelekezo ya Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe.
Humprey Polepole (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo yenye lengo la
kukagua utekelezaji wa majukumu ya TPSC.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza
na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (hawapo
pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo katika Chuo cha Utumishi wa
Umma yenye lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya chuo hicho.
Baadhi
ya watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Dar es Salaam
wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za
Mitaa, Mhe. Humprey Polepole (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo
yenye lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya TPSC.
Mjumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Saashisha
Mafue ambaye ni mnufaika wa mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma
akitoa ushuhuda wa namna alivyopata mafunzo katika chuo hicho wakati wa ziara
ya kikazi ya kamati hiyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya
TPSC.
Mtendaji
Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Dkt. Emmanuel Shindika
akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya chuo chake kwa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo
yenye lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya TPSC.
No comments:
Post a Comment