Wednesday, September 30, 2020

SERIKALI KUSIMAMISHA MISHAHARA YA MAAFISA UTUMISHI WATAKAOSABABISHA WATUMISHI KUTOLIPWA MISHAHARA

 Na. James Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 30 Septemba, 2020.

Maafisa Utumishi watakaozembea na kusababisha Watumishi wa Umma nchini kutolipwa mishahara yao kwa wakati, watasimamishiwa mishahara na Serikali mpaka watakapohakikisha watumishi hao wamelipwa mishahara yao.

Hayo yamesemwa jana na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael wakati akifungua mafunzo ya wiki mbili ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara kwa kundi la pili la Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 140 kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Kigoma na Tabora yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.

DKt. Michael amesema, kuna tatizo katika baadhi ya Taasisi za Umma kwani wapo Maafisa Utumishi wanajifanya miungu watu wakati wajibu wao ni kumtengenezea mazingira mazuri ya kikazi mtumishi ili ajisikie yuko sehemu salama na aweze kutekeleza ipasavyo jukumu la kuwahudumia wananchi.

“Msiwafanye watumishi mnaowasimamia kuona sehemu ya kazi kama jehanamu, hivyo mbadilike kwani Serikali haitomvumilia yeyote atakaye kinzana na azma yake ya kuboresha huduma kwa wananchi”, Dkt. Michael alisisitiza.

Ameongeza kuwa, ni lazima Maafisa Utumishi wabadilike kwa kuwajengea mazingira Watumishi wa Umma kuipenda Serikali yao kwasababu inawajali na kuthamini mchango wao katika maendeleo ya taifa.

Dkt. Michael amefafanua kuwa, Serikali inamhakikishia mtumishi usalama wa ajira yake tofauti na sekta binafsi, hivyo hakuna Afisa Utumishi atakayevumiliwa pindi akisababisha Serikali kulaumiwa na Watumishi wa Umma au Wananchi.

Naye, Mkuu wa Idara ya Utawala na Utumishi, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Bw. Boniface B. Chatila kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, ameahidi kuwa, wakirejea katika maeneo yao ya kazi watahakikisha wanatekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuondoa kero ya Watumishi wa Umma kufuata huduma Ofisi ya Rais Utumishi Dodoma, huduma ambazo wanastahili kupewa katika maeneo yao ya kazi.

Aidha, Bw. Chatila amemhakikishia Dkt. Michael kuwa, ujuzi watakaoupata kupitia mafunzo ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara watautumia ipasavyo kuongeza ufanisi kiutendaji ili kuboresha utoaji huduma kwa umma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, ACP Ibrahim Mahumi amesema, suala la mtumishi kukosa mshahara hivi sasa linachukuliwa kama ni kosa kubwa hivyo Afisa Utumishi atakayebainika atasimamishiwa mshahara ikiwa ni hatua ya awali na atachukuliwa hatua za kinidhamu ikizingatiwa kuwa, mfumo mpya utaonesha uzembe wa afisa huyo.

Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara utaanza kutumika rasmi Mwezi Novemba, 2020 mara baada ya kukamilika kwa mafunzo ya makundi yote ya Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala ambao ndio wenye jukumu la kuutumia mfumo huo kiutendaji.

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael akizungumza na washiriki wa mafunzo ya wiki mbili ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara kwa kundi la pili la Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 140 yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.


Baadhi ya Washiriki wa mafunzo ya wiki mbili ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara kwa kundi la pili la Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 140 wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael wakati akifungua mafunzo hayo yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.


Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, ACP Ibrahim Mahumi akitoa ufafanuzi wa utekelezaji wa maelekezo ya Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael aliyoyatoa wakati akifungua mafunzo ya kundi la pili la Maafisa Utumishi na Maafisa Utawala 140 yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.



Mkuu wa Idara ya Utawala na Utumishi, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Bw. Boniface B. Chatila akiahidi kutekeleza maelekezo ya Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa niaba ya kundi la pili la  washiriki 140 wa mafunzo ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.


Sunday, September 27, 2020

MFUMO MPYA WA KITANZANIA WA TAARIFA ZA KIUTUMISHI NA MISHAHARA KUDHIBITI UINGIZWAJI WA TAARIFA ZISIZO SAHIHI

 

James Mwanamyoto – Dodoma

Tarehe 27 Septemba, 2020

Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 108 waliohitimi Mafunzo ya siku 12 ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara wametakiwa kukamilisha usahihishaji wa taarifa za watumishi zilizopo kwenye mfumo wa sasa ili ziweze kuingizwa katika mfumo mpya, kwani mfumo mpya hautoruhusu kuingiza taarifa ambazo sio sahihi na zisizokamilika.

Maelekezo hayo yametolewa jana jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Cosmas Ngangaji wakati akifunga mafunzo hayo yaliyokuwa na lengo la kuboresha utendaji kazi na usimamizi wa rasilimaliwatu na mishahara.

Bw. Ngangaji amesema, baada ya kukamilika kwa mafunzo haya na kuanza kutumika rasmi kwa mfumo huu mpya, Serikali inatarajia mfumo mpya utatumika kutatua kero za watumishi kwa ufanisi na kwa haraka zaidi ikiwa ni pamoja na kuwaondolea usumbufu wa kufuata huduma Ofisi ya Rais Utumishi.

Bw. Ngangaji ameongeza kuwa, mfumo mpya utaongeza uadilifu kiutendaji kwani umewezeshwa kurekodi matukio yote yatakayokuwa yakifanywa na Maafisa waliopewa dhamana ya kutumia Mfumo huo.

“Serikali kupitia mfumo huu itakuwa ikifuatilia na kujua ni Afisa yupi amefanya nini au amekusudia kufanya nini, wapi na muda gani? Bw. Ngangaji amefafanua.

Aidha, Bw. Ngangaji amesema mfumo mpya utaimarisha uwajibikaji na kuwawezesha watumishi kufuatilia utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kiutumishi yanayowahusu kupitia simu na barua pepe hivyo, kuongeza uwajibikaji na kujiepusha kufanya kazi kwa mazoea.

“Watumishi wa Umma watakuwa wakipata taarifa na kujua kama kazi iliyofanyika bado ipo kwa Afisa Utumishi, Mwajiri au imeshatumwa UTUMISHI kwa ajili ya kuidhinishwa,” Bw. Ngangaji amesisitiza.

Naye, Mkuu wa Idara ya Utawala, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Bw. Martin Ndilanha kwa niaba ya washiriki wa mafunzo amemhakikisha Bw. Ngangaji kuwa, wamepata mafunzo bora ya mfumo mpya na kuwa wabobezi katika kuutumia ili kuondoa kero na changamoto zilizokuwa zikiwakabili Watumishi wa Umma nchini.

Bw. Ndilanha amesema, Mfumo huo mpya ulioboreshwa unapunguza uzalishaji wa madeni kwa Serikali, unarahisisha na kupunguza gharama za uandaji wa bajeti ya Serikali hivyo wako tayari kuutumia ipasavyo.

Serikali imepanga kuanza matumizi rasmi ya mfumo huu mpya mwezi Novemba, 2020 baada ya kukamilisha mafunzo kwa makundi manne ya Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2020.


Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Cosmas Ngangaji akifunga mafunzo ya siku 12 ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara kwa Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 108 (hawapo pichani) kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro yaliyofanyika katika Ukumbi wa VETA jijini Dodoma.

Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya siku 12 ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara kwa Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 108 kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Cosmas Ngangaji (hayupo pichani) wakati akifunga mafunzo hayo katika Ukumbi wa VETA jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Bw. Priscus Kiwango akimkaribisha Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Cosmas Ngangaji kufunga mafunzo ya siku 12 ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara kwa Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 108 (hawapo pichani) kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro katika Ukumbi wa VETA jijini Dodoma.


Mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara akipokea cheti kutoka kwa Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Cosmas Ngangaji baada ya kufunga mafunzo hayo katika Ukumbi wa VETA jijini Dodoma.



Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala, Halmasauri ya Wilaya ya Chemba, Bw. Martin Ndilanha ambaye ni miongoni mwa wahitimu wa mafunzo ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara akitoa neno la shukrani kwa Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Cosmas Ngangaji mara baada ya kufungwa kwa mafunzo hayo katika Ukumbi wa VETA jijini Dodoma.


Friday, September 25, 2020

SHERIA YA SERIKALI MTANDAO KUTEKELEZWA KIKAMILIFU NA TAASISI ZA UMMA

 Na. James Mwanamyoto-Dodoma

25 Septemba, 2020

Katika kukabiliana na changamoto zinazohusiana na suala la usalama wa taarifa za Serikali na mifumo ya TEHAMA ya utoaji huduma kwa umma, Serikali imeziagiza Taasisi zote za Umma kuhakikisha zinatekeleza kikamilifu Sheria ya Serikali Mtandao namba 10 ya Mwaka 2019 na Kanuni zake ambayo imetungwa kwa lengo la kusimamia matumizi ya Serikali Mtandao.

Agizo hilo limetolewa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu, ACP Ibrahim Mahumi kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati akifungua mafunzo kwa Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa Sheria ya Serikali Mtandao .

ACP Mahumi amesema, umakini katika suala zima la usalama mitandaoni na kwenye mifumo unahitajika ili kuunga mkono jitihada za Serikali kuboresha huduma kwa umma kwa njia ya Serikali Mtandao.

Ameongeza kuwa, kila Taasisi inalo jukumu la kuwaelimisha watumishi wake ili wawe na uelewa wa pamoja wa namna ya kutekeleza Sheria ya Serikali Mtandao pamoja na kanuni zake kwa lengo la kuepuka athari zitakazoweza kujitokeza kwa kutokuzingatia sheria hiyo.

“Watu wa TEHAMA kazi yenu kubwa ni kurahisisha utendaji kazi Serikalini hivyo, naamini mafunzo haya yatawasaidia kuhimiza utekelezaji wa Sheria ya Serikali Mtandao na kufanya maboresho kwenye mifumo ya TEHAMA ya utoaji huduma inayotumiwa na Taasisi zenu,” ACP Mahumi amesisitiza.

Kwa kuzingatia umuhimu wa utoaji huduma bora kwa umma, ACP Mahumi ameziasa Taasisi za Serikali ambazo zinasuasua kutumia Serikali Mtandao kuhakikisha zinatumia fursa ya uwepo wa Serikali Mtandao ili wananchi wanufaike na huduma.

Sheria ya Serikali Mtandao Namba 10 ya mwaka 2019 ilianza kutumika rasmi tarehe 15 Disemba, 2019 baada ya kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo iliiwezesha iliyokuwa Wakala ya Serikali Mtandao kuwa Mamlaka. 

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu, ACP Ibrahim Mahumi akifungua mafunzo ya siku moja kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa Sheria ya Serikali Mtandao kwa Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini  kwa niaba Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, yaliyofanyika leo jijini Dodoma.


Baadhi ya washiriki wakimsikiliza Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu, ACP Ibrahim Mahumi (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo ya siku moja kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa Sheria ya Serikali Mtandao kwa Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini yaliyofanyika leo jijini Dodoma.



Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Bw. Priscus Kiwango akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo ya siku moja kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa Sheria ya Serikali Mtandao kwa Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini yaliyofanyika leo jijini Dodoma.


Monday, September 14, 2020

MFUMO MPYA WA HCMIS KUHIFADHI TAARIFA MUHIMU ZA KIUTUMISHI NA KUTATUA CHANGAMOTO ZA MADAI YA MALIMBIKIZO YA MISHAHARA

 

Na James Mwanamyoto- Dodoma

Tarehe 14 Septemba, 2020

Mfumo mpya wa Taarifa Shirikishi za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) uliotengenezwa na wataalam wa ndani una uwezo wa kuhifadhi taarifa muhimu za Watumishi wa Umma tangu kuajiriwa kwao na utatatua changamoto nyingi za kiutumishi ikiwamo ya madai ya muda mrefu ya malimbikizo ya mishahara.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael wakati akifungua Mafunzo ya Mfumo Mpya wa HCMIS kwa kundi la kwanza linalojumuisha Maafisa Utumishi Utawala kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini Dodoma.

Dkt. Michael amesema Mfumo huo pamoja na kujumuisha taarifa zote muhimu zinazohusu maendeleo ya Mtumishi wa Umma tangu aajiriwe hadi anapofikia ukomo wa ajira yake, pia unajumuisha taratibu zote muhimu za kiutendaji katika Utumishi wa Umma.

“Tofauti na Mfumo wa Lawson unaotumika hivi sasa, Mfumo huu mpya unahifadhi taarifa za Miundo ya Taasisi za Umma, Miundo ya Maendeleo ya Utumishi, Miundo ya Mishahara ya Watumishi, Ikama na Bajeti, taarifa za Ajira za Watumishi na matukio yote yanayowahusu, malipo ya mishahara yao, makato ya marupurupu yao kwa kila mwezi na upandishwaji vyeo,” Dkt. Michael amefafanua.

Dkt. Michael ameainisha kuwa, Mfumo mpya utaondoa changamoto ya madai ya malimbikizo ya mshahara ya muda mrefu pindi Mtumishi anapopandishwa cheo, kwani mara baada ya kupanda cheo, taarifa zake zitabadilishwa kwa wakati ikiwa ni pamoja na kupata mshahara mpya.

Naibu Katibu Mkuu huyo amesisitiza kuwa, Mfumo huo uliotengenezwa na wataalam wa ndani wa Serikali, unaakisi mahitaji ya ndani ya Serikali, utaimarisha usalama wa taarifa na nyaraka pamoja na kupunguza gharama za matengenezo na ulipiaji leseni ambapo Serikali ilikuwa ikitumia dola 217,000 kwa mwaka ambazo  hivi sasa zitatumika katika miradi ya maendeleo nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Washiriki wa mafunzo hayo, Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala, Wilaya ya Kondoa, Bw. Archanus Kilaja, ameipongeza Serikali kutengeneza Mfumo kwa kutumia wataalam wa ndani, kitendo kinachoashiria nchi yetu imeanza kujitegemea kwenye eneo la mifumo.

Bw. Kilaja ameahidi kuyafanyia kazi mafunzo watakayoyapata ili watakaporejea kwenye maeneo yao ya kazi waweze kuutumia mfumo vizuri kama Serikali ilivyokusudia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Priscus Kiwango amesema, Mafunzo yatakayotolewa kwa kundi la kwanza la Maafisa Utumishi na Utawala, yamepewa muda mrefu wa wiki mbili kwani ndio walengwa wakuu na watumiaji wa mfumo, muda huo utawawezesha kufahamu vizuri namna mfumo unavyofanya kazi.

Bw, Kiwango ameongeza kuwa, Mfumo mpya ambao utatumika badala ya Mfumo wa Lawson unaotumika hivi sasa, umeshafanyiwa majaribio, na Serikali imejiridhisha kwamba uko tayari kwa ajili ya kuanza kufanya kazi rasmi na utakuwa bora zaidi ya unaotumika sasa.

Maandalizi ya Mfumo Mpya wa HCMIS ulianza mwaka 2018 kwa kukusanya mahitaji ya wadau kutoka kwenye taasisi mbalimbali za Serikali, usanifu na ujenzi wa Mfumo ulianza mwaka 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2020.


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akifungua Mafunzo ya Mfumo Mpya wa HCMIS kwa kundi la kwanza linalojumuisha Maafisa Utumishi Utawala kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro yaliyofanyika leo kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini Dodoma. 



Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya Mfumo Mpya wa HCMIS kwa kundi la kwanza linalojumuisha Maafisa Utumishi Utawala kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro wakimsikiliza  Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael wakati akifungua Mafunzo hayo leo kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini Dodoma. 


Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Priscus Kiwango akitoa neno la utangulizi kuhusiana na mafunzo ya Mfumo Mpya wa HCMIS yaliyofunguliwa na  Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini Dodoma leo. 


Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala, Wilaya ya Kondoa, Bw. Archanus Kilaja, akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Washiriki wa Mafunzo ya Mfumo Mpya wa HCMIS mara baada ya Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael kufungua Mafunzo leo kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini Dodoma. 

 

 

Thursday, September 10, 2020

SERIKALI KUTOA MWONGOZO WA UJUMUISHAJI WA MASUALA YA JINSIA KATIKA UTUMISHI WA UMMA ILI KUONGEZA TIJA KIUTENDAJI

 Na. Aaron Mrikaria-Dodoma

Tarehe 10 Septemba, 2020

Serikali imeandaa Rasimu ya Mwongozo wa Ujumuishaji wa Masuala ya Jinsia katika Utumishi wa Umma ambao utatoa maelekezo ya namna ya kujumuisha masuala ya kijinsia mahala pa kazi na kujenga mazingira bora na wezeshi kwa makundi mbalimbali kwenye taasisi za umma, ili mwongozo huo uwe ni chachu ya kuongeza tija kiutendaji kwa Watumishi wa Umma na Serikali kwa ujumla.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili kilichohudhuriwa na Wakurugenzi wa Wizara zote kilichojadili na kutoa mapendekezo ya kuboresha rasimu hiyo, kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini DODOMA.

Dkt. Michael amewasititiza waajiri kuwa, pendekezo la urithishanaji madaraka kuzingatia suala la kijinsia lipewe umuhimu mkubwa katika utekelezaji wake, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanawake wanapata fursa kujumuishwa kwenye mipango ya mafunzo ili kujengewa uwezo kiutendaji.

Licha ya kuafiki pendekezo la kutilia mkazo haja ya wanawake kupewa kipaumbele katika nafasi za uongozi na kuwekewa mazingira wezeshi katika utekelezaji wa majukumu yao mahala pa kazi, Dkt. Michael pia amehimiza umuhimu wa rasimu hiyo kuyawezesha makundi yote kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi katika Utumishi wa Umma.

Aidha, Dkt. Michael awetaka viongozi katika Utumishi wa Umma kuhakikisha wanabaini watumishi wenye vipaji maalum kutoka makundi anuai na kuviendeleza vipaji hivyo, pamoja na kuangalia namna ya kuanzisha vituo vya malezi kwa watoto katika majengo ya Ofisi za Umma ili mtumishi anayenyonyesha aweze kutumia muda wake kikamilifu katika kutekeleza majukumu ya kikazi.

Naye, Mkurugenzi Msaidizi Anuai za Jamii, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Leila Mavika, amesema tofauti na Mwongozo wa mwaka 2010, rasimu hii inayoboreshwa imezingatia masuala ya jinsia na usimamizi wa rasilimaliwatu, hivyo muongozo huu ukiidhinishwa rasmi kutumika utakuwa ni mahususi kuratibu ujumuishwaji wa masuala ya jinsia katika usimamizi wa rasilimaliwatu kwenye Utumishi wa Umma.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akizungumza na washiriki wa kikao kazi cha siku mbili kilichojadili na kutoa mapendekezo ya kuboresha Rasimu ya Mwongozo wa Ujumuishaji wa Masuala ya Jinsia katika Utumishi wa Umma, kabla ya kufunga rasmi kikao kazi hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini DODOMA jana jioni.

Mmoja wa washiriki (aliyesimama) wa  kikao  kazi cha siku mbili kilichojadili na kutoa mapendekezo ya kuboresha Rasimu ya Mwongozo wa Ujumuishaji wa Masuala ya Jinsia katika Utumishi wa Umma akitoa mchango wake katika kikao kazi hicho, kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini DODOMA jana jioni.


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao kazi cha siku mbili kilichojadili na kutoa mapendekezo ya kuboresha Rasimu ya Mwongozo wa Ujumuishaji wa Masuala ya Jinsia katika Utumishi wa Umma, mara baada ya kufunga rasmi kikao kazi hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini DODOMA jana jioni.

Friday, September 4, 2020

TAIFA LITAJENGWA NA WANANCHI KUSHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA

Na. Mary Mwakapenda-Ngorongoro

Tarehe 04 Septemba, 2020 

Watanzania wameaswa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa kwa kuzitumia vizuri Ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini ili kuwa chachu ya maendeleo kwenye jamii wanayoishi, ikizingatiwa kuwa rushwa ikishamiri katika taifa lolote lile huwa ni kikwazo kikubwa cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika wakati akiwasihi wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro kuitumia vizuri Ofisi ya TAKUKURU wilayani humo, aliyoizindua rasmi Septemba 4, 2020.

Mhe. Mkuchika amesema, njia sahihi ya kuleta maendeleo nchini ni ushiriki wa kila Mtanzania kuwafichua wala rushwa na kutoshiriki vitendo vya rushwa, hususani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ambao taifa linategemea kupata viongozi bora wenye nia ya dhati ya kuleta maendeleo.

Msishawishike kuomba rushwa wala kupokea rushwa kwa lengo la kumchagua kiongozi wa chama chochote kile cha siasa”, Mhe. Mkuchika amewaasa wananchi na kuongeza kuwa, uchaguzi ukigubikwa na vitendo vya rushwa hautakuwa na tija kwa maendeleo ya taifa.

Aidha, kuhusu azma ya Serikali kuokoa fedha za umma, Mhe. Mkuchika ameipongeza TAKUKURU Mkoa wa Arusha kwa kuokoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 2,490,396,226.00 katika kipindi cha mwaka 2019/2020, fedha ambazo zitatumika kikamilifu kwenye miradi ya maendeleo.

Kama mnavyofahamu mtazamo wa mataifa kwa sasa ni kurejesha Serikalini mali zilizopatikana kwa njia ya rushwa na ubadhirifu ili zitumike kwenye shughuli za maendeleo.” Mhe. Mkuchika amefafanua.

Mhe. Mkuchika ameahidi kuwa, Serikali itahakikisha TAKUKURU inaendelea kuimarika, hivyo amewataka Watumishi wa TAKUKURU kuongeza juhudi katika kutekeleza jukumu lao la kuzuia na kupambana na rushwa nchini.

Akitoa maelezo ya awali, Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bibi Sabina Seja amemshukuru Mhe. Rais kwa kuwajengea ofisi na kuwapatia rasilimali za kutosha, hivyo ameahidi kuwa TAKUKURU itafanya kazi kwa bidii kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa nchini.

Ufunguzi wa jengo la Ofisi ya TAKUKURU Ngorongoro ni ushahidi wa namna Serikali ilivyodhamiria kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kwa kuiwezesha TAKUKURU kuwa na ofisi itakayorahisisha utendaji kazi wake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika akizungumza na Watumishi na wananchi wilayani Ngorongoro kabla ya kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro Septemba 04, 2020.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika akikata utepe kufungua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro Septemba 04, 2020. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Rashid Taka na kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,Bibi Sabina Seja.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika akizindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro Septemba 04, 2020.

Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,Bibi Sabina Seja akitoa maelezo ya awali kuhusu jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika kuzungumza na wananchi na kulizindua jengo hilo Septemba 04, 2020.

Baadhi ya Watumishi na wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika alipokuwa akizungumza nao kabla ya kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilayani humo Septemba 04, 2020.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika akizungumza na Viongozi wa Wilaya ya Ngorongoro ofisini kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Rashid Taka (wa kwanza kulia kwa Mhe. Waziri) alipoitembelea Ofisi hiyo kabla ya kufungua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro Septemba 04, 2020.










Thursday, September 3, 2020

OPERESHENI ZA TAKUKURU MKOANI SINGIDA ZAOKOA SHILINGI 199,559,254/= IKIWEMO MIKOPO UMIZA

Na. Mary Mwakapenda-Manyoni

Tarehe 03 Septemba,2020

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imefanikiwa kuokoa kiasi cha Tsh. 199,559,254/= kufuatia operesheni mbalimbali zilizofanywa ili kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa mkoani humo katika kipindi cha kuanzia Julai 2019 hadi Juni 2020.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika wakati akimkaribisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Mhe. Mkuchika ameyataja baadhi ya maeneo ambayo operesheni hiyo iliyalenga kuwa ni pamoja na mikopo umiza ambapo kiasi cha Tsh. 58,150,000/= kiliokolewa, kwa upande wa mapato yatokanayo na usimamizi wa madini, kiasi cha Tsh. 44,623,254/= kiliokolewa, sanjari na hayo, kiliokolewa kiasi cha Tsh. 11,456,500/= kutokana na mapato ya usimamizi wa minada, na kiasi cha Tsh. 85,329,500/= kilirudishwa kutoka kwa wanachama wa vyama vya ushirika.

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, jitihahada zote hizi zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na TAKUKURU zinatokana na weledi, ujasiri na uzalendo uliopo katika kushughulikia tatizo la rushwa nchini, hivyo ameitaka TAKUKURU kuendelea na kasi hiyo ili kudhibiti vitendo vya rushwa na ufisadi nchini.

Katika eneo la utoaji elimu dhidi ya vitendo vya rushwa, Mhe. Mkuchika ameanisha kuwa, TAKUKURU imefanikiwa kufungua na kuimarisha klabu 234 za Wapinga Rushwa mashuleni na vyuoni na kutoa semina pamoja na mikutano ya hadhara 225.

Aidha, Mhe. Mkuchika amemuahidi Mhe. Ndugai kujenga Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Kongwa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa tarehe 22 Julai, 2020 wakati akifungua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Chamwino na kuongeza kuwa, hatua hii inadhirisha nia ya dhati ya Serikali ya kupambana na vitendo vya rushwa nchini.

Jengo la Ofisi ya TAKUKURU la Wilaya ya Manyoni ni mojawapo ya majengo saba ambayo Mhe. Rais Magufuli alitakiwa kuyafungua kwa pamoja tarehe 22 Julai, 2020 wakati akifungua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Chamwino, Dodoma. Hata hivyo, aliweka utaratibu wa kuyafungua kwa nyakati tofauti na kumuelekeza Mhe. Ndugai kulifungua jengo hilo. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George Mkuchika akitoa maelezo kuhusu jengo la TAKUKURU Wilaya ya Manyoni kabla ya kumkaribisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai kuzungumza na wananchi na kulizindua jengo hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George Mkuchika akimkaribisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai kuzungumza na wananchi kabla ya kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai akizungumza na wananchi wilayani Manyoni  kabla ya kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai (kushoto) akisoma kibao cha ufunguzi wa jengo baada ya kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Manyoni mkoani Singida jana. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George Mkuchika na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Bibi Rahabu Magwisa.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George Mkuchika akiipongeza Klabu ya Wapinga Rushwa ya Shule ya Sekondari ya Mlewa Wilayani Manyoni wakati wakiimba wimbo wa mapambano dhidi ya rushwa kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Wednesday, September 2, 2020

WATUMISHI OFISI YA RAIS-UTUMISHI WAPATIWA MAFUNZO KUONGEZA WELEDI NA UFANISI ILI KUBORESHA UTOAJI HUDUMA

 Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 02 Septemba, 2020.

Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUUB) wapatiwa mafunzo yatakayowawezesha kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na ufanisi ili kuboresha utoaji huduma kwa umma na wadau wengine wa masuala ya kiutumishi na utawala bora.

Hayo yamesemwa leo na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wa ofisi yake yatakayotoa fursa ya kuwajengea uwezo kwenye eneo la uandishi wa nyaraka za ofisi, utunzaji bora wa kumbukumbu na nyaraka, mapambano dhidi ya rushwa ikiwa ni pamoja na namna bora ya kukabiliana na msongo wa mawazo mahala pa kazi.

Dkt. Michael amewaka watumishi hao kufuatilia kwa umakini mafunzo hayo ili wapate elimu na weledi kuhusu namna bora ya uandishi wa nyaraka, utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, kuepuka vitendo vya rushwa na msongo wa mawazo ambavyo kwa kiasi kikubwa vinaweza kuathiri utendaji kazi wao wa kila siku.

“Mafunzo haya ni muhimu katika kuiwezesha ofisi kupata watumishi mahiri, waadilifu, wenye kuzingatia weledi na ufanisi kiutendaji”, Dkt. Michael amesisitiza.

Dkt. Michael amefafanua kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kama zilivyo taasisi nyingine nyeti, inapaswa kuwa na watumishi bora na wenye ujuzi na maarifa yatakayowaongezea ufanisi kiutendaji na ndio maana menejimenti imeamua kuwapatia mafunzo yatakayowajengea uwezo wa kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau wengine.

Mafunzo haya ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi wa OR-MUUUB yanafanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kuanzia tarehe 02 hadi 04/09/2020 na yatahudhuriwa na watumishi 218.



Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael akifungua mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wa ofisi yake (hawapo pichani) yenye lengo la kuwajengea uwezo kiutendaji ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau wa masuala ya kiutumishi na utawala bora.

Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifurahia ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa uandishi wa nyaraka za ofisi, utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, mapambano dhidi ya rushwa pamoja na namna bora ya kukabiliana na msongo wa mawazo mahala pa kazi.

Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Mwanaheri Cheyo akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa ofisi hiyo yaliyoanza Septemba 2, 2020 katika Ukumbi wa UDOM na yatahitimishwa Septemba 4, 2020.