Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah Kairuki (Mb), amewataka Watendaji wa Taasisi za Serikali kuwashirikisha watumishi katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na nyaraka mbalimbali zinazotolewa na Serikali ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Waziri Kairuki aliyasema hayo alipokuwa akiongea na watumishi wa mkoa wa Tanga katika kikao kazi na watumishi hao kilichofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Mhe. Kairuki amesema ni vema watumishi wakashirikishwa katika nyaraka hizo muhimu ili waweze kujua nini kinaendelea katika Serikali yao wakiwa kama watumishi wa umma.
“Nyaraka hizi zimetengenezwa kwa ajili yao hivyo kukaa kimya bila kuwashirikisha si sawa kwani nao wanapaswa kujua ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo,” Mhe. Kairuki aliongeza.
Amesema kumekuwa na mabadiliko mengi katika miundo lakini watumishi hawafahamu kwasababu hawashirikishwi.
Aidha, Mhe. Kairuki amewataka Watendaji hao kutenga muda angalau mara moja kwa mwezi ili kusikiliza malalamiko na kero za watumishi.
“Watumishi wengi wamekuwa wakinyanyasika sana lakini wanashindwa pa kusemea hivyo ni vema tukatenga muda wa kusikiliza wanakumbwa na changamoto zipi,” aliongeza.
Ameongeza kuwa kusikiliza kero za watumishi mara kwa mara kutasaidia kupunguza malalamiko mengi na watumishi kufanya kazi kwa bidii hivyo kuongeza pato la taifa.
Ziara ya Mhe. Kairuki mkoani Tanga, ni mwendelezo wa utaratibu aliojiwekea wa kukutana na watumishi katika mikoa mbalimbali nchini kusikiliza kero na malalamiko ili kuweza kuyafanyia kazi. Kabla ya kukutana na watumishi wa Mkoa wa Tanga, Mhe, Kairuki ameshakutana na watumishi wa mikoa ya Singida, Dodoma, Kilimanjaro, Arusha, Manyara.
No comments:
Post a Comment