Timu ya netiboli ya Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma imeanza mashindano ya SHIMIWI 2014 kwa
kuifunga timu ya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika magori 57 dhidi ya 18.
Ikicheza kwa kujiamini ndani
ya Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro iliwachukua takribani sekunde 7 kufunga
goli la kwanza kupitia kwa mchezaji Monica Aloyce (GS) lililoamsha shangwe na
ndelemo kwa wapenzi wa mchezo huo.
Ustadi wa Monica Aloyce (GS)
aliyefunga magori 16 kwa kushirikiana na Anna Msulwa (GA) aliyefunga
magori 9 uliisaidia Utumishi kupata
magori 25 dhidi ya matano (5) ya kilimo katika kipindi cha kwanza cha mchezo
huo.
Kipindi cha pili kilianza
kwa kasi hali iliyopelekea kocha wa Utumishi kumpumzisha mchezaji Monica Aloyce
(GS) na nafasi yake kuchukuliwa na Fatuma Machenga (GS) aliyebadilisha hali ya
mchezo kwa kufunga magori 27.
Akizungumza mara baada ya
mchezo kumalizika,kocha wa Wizara ya kilimo Bi. Rabia Mohamed alikiri kuwa timu
yake ilikuwa na mapungufu kwenye safu ya Ulinzi hali iliyopelekea timu yake
kupoteza mchezo.
“Timu yangu haikucheza
vizuri kwenye safu ya ulinzi hivyo nitafanya marekebisho ya mapungufu
yaliyojitokeza ili tupate ushindi katika mechi inayofuata” alisema Bi. Rabia.
Naye,kocha wa Utumishi Bw.
Methew Kambona aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri kwa kiwango
kinachoridhisha,aidha Bw. Kambona alisema kuwa timu yake imejipanga vizuri na
kuhaidi kuibuka kinara katika mashindano hayo.
No comments:
Post a Comment