Wachezaji wa timu ya Utumishi wakiwadhibiti
wachezaji wa Mahakama wasifunge katika goli lao katika mchezo wa SHIMIWI
uliochezwa katika uwanja wa Jamhuri.
|
Timu ya Mpira wa Pete ya Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma imeifungashia virago katika mashindano ya
SHIMIWI timu ya Mahakama kwa ushindi wa Pete
56 dhidi ya 14.
Utumishi iliibuka na ushindi huo mkubwa
katika mechi za hatua ya kumi na sita bora ambapo mshindi husonga mbele.
Kwa ushindi huo, Utumishi imefanikiwa
kuingia robo fainali katika mchezo utakaochezwa kesho kwa kupambana na jirani
zake Hazina.
Mchezo ulioiwezesha Utumishi kutinga robo
fainali uliongezwa makali na wachezaji wake Fatuma Machenga (GS) aliyewashushia
Mahakama mvua ya Pete 26, akifuatiwa na Anna Msulwa (GA) aliyefunga Pete 4
hivyo kuhitimisha nusu ya kwanza kwa idadi ya Pete 30 dhidi ya 7 za Mahakama.
Kipindi cha pili mambo yaliiendea mrama Mahakama kwa kuzidiwa kila hali ambapo
Utumishi ilizidi kuibugiza magoli. Ushirikiano wa Wachezaji Fatuma Machenga
(GS) na Anna Msulwa (GA) uliitupa Mahakama nje ya mashindano kwani hadi kipenga
cha mwisho wachezaji hao walishaandika ushindi mnono kila mmoja akifunga Pete
47 na 9, hivyo Utumishi kuibuka mshindi kwa jumla ya Pete 56 dhidi ya 14 za
Mahakama.
Mara baada ya filimbo ya mwisho, mchezaji
wa Mahakama Veronica Ndasi (GK) alikubali kuwa timu yao ilizidiwa kimchezo “
wapinzani wetu wako vizuri zaidi kimchezo na wametutoa”.
Ndasi alisema Utumishi walijiandaa vizuri
hata hivyo nao Mahakama walitoa upinzani kimchezo hivyo mashabiki wasikate
tamaa.
Kapteni wa Utumishi Elizabeth Fusi (C)
aliwapongeza wachezaji wenzake na kuahidi kuendeleza kipigo hicho hicho kwa
timu ya Hazina katika mchezo wa robo fainali.
Mashindano ya 38 ya SHIMIWI yanayowahusisha
watumishi wa Serikali katika michezo tofauti tofauti yanafanyika mkoani
Morogoro katika viwanja mbalimbali.
No comments:
Post a Comment