Wednesday, October 15, 2014

UTUMISHI BINGWA MPYA MPIRA WA PETE SHIMIWI 2014

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Utumishi Bw. HAB Mkwizu akimkabidhi kapteni wa Utumishi Bi. Elizabeth Fusi kombe la mshindi wa kwanza mpira wa pete siku ya kilele cha mashindano ya SHIMIWI 2014 uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mh. Joel Bendera na viongozi wa SHIMIWI Taifa wakishuhudia.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Utumishi Bw. HAB Mkwizu akimkabidhi kombe mshindi wa kwanza wa mbio za baiskeli kwa wanaume kutoka Utumishi Bw. Hassan Ligoneko (kulia) siku ya kilele cha mashindano ya SHIMIWI 2014 uwanja wa Jamhuri, Morogoro. 

Wachezaji wa Ofisi ya Rais Utumishi wakiwa katika maandamano huku wakipunga mkono kwa mgeni rasmi siku ya kilele cha mashindano ya SHIMIWI 2014 uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Timu ya mpira wa Pete ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma imetawazwa rasmi kuwa bingwa kwa Mashindano ya 38 ya SHIMIWI kwa mwaka 2014.
Utumishi imefanikiwa kuwa bingwa baada ya kuisambaratisha timu Wizara ya Afya kwa ushindi mnono wa Pete 65 kwa 35 katika mchezo uliochezwa katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Katika mchezo huo, wachezaji Fatuma Machenga (GS) na Anna Msulwa (GA) wa Utumishi wakicheza kwa ushirikiano waliliongoza jahazi la Utumishi na kufanikisha ushindi huo mnono. Machenga (GS) alifanikiwa kufunga 45 na Msulwa (GA) 20 hivyo kuhakikisha Utumishi inakua bingwa.
Mara baada ya mchezo kumalizika, kocha wa timu ya Afya Mwajuma Kisengo alisema mchezo ulikuwa mzuri na wenye ushindani ila bahati haikua yao na wanasubiri mashindano yajayo.
“Mimi kama kocha na mwamuzi wa kimataifa nawapongeza wachezaji wangu na wenzao wa Utumishi, pamoja na waamuzi ambao wamechezesha vizuri kwa kuzingatia sheria za mchezo huu” Kisengo alisema.
Naye kocha wa Utumishi Bw. Methew Kambona aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri na kunyakua kombe la SHIMIWI 2014.
Utumishi ilifuzu hatua ya fainali baada ya kuifungashia virago Ikulu ambao walikuwa mabingwa watetezi kwa jumla ya magoli 42 dhidi ya 41 kwenye mchezo wa nusu fainali uliopigwa jana katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.


No comments:

Post a Comment