Wednesday, May 14, 2025

SERIKALI KUANDAA DAFTARI LA HUDUMA ZA SERIKALI LITAKALOWEZESHA WANANCHI KUPATA HUDUMA KATIKA CHANZO KIMOJA

 


Na Eric Amani-Morogoro

 

Serikali inaandaa Daftari la Huduma za Serikali litakalowezesha wananchi kupata taarifa muhimu za huduma zote zinazotolewa na Serikali katika chanzo kimoja.

 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini Bw. Priscus Kiwango wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa Wawezeshaji wa Daftari la Huduma za Serikali (Government Services Directory - GSD katika Taasisi za Serikali yalioanza jana Mkoani Morogoro.

 

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu UTUMISHI, Bw. Kiwango amesema, Serikali pia imejikita katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa wananchi, hivyo Daftari hilo ambalo ni la Kielektroniki na huduma ambazo tayari zinatolewa kielektroniki katika Taasisi, zitapatikana kieletroniki kupitia Daftari hilo.

 

 “Kama tunavyofahamu, Serikali ina jukumu kubwa la kuhakikisha inatoa huduma bora kwa wananchi kupitia Taasisi mbalimbali za Serikali, hivyo ili  kufikia azma hiyo, inaandaa Daftari hilo kurahisisha upatikanaji wa huduma za Serikali,” amesema.

 

Amesema lengo kuu la Daftari hilo ni kuhakikisha huduma za Serikali zinakuwa wazi, zinapatikana kwa urahisi na zinatolewa kwa viwango vya ubora unaokubalika.

 

Amesema kupitia Daftari hilo, wananchi wataweza kujua huduma zipi zinatolewa na Taasisi gani na wapi, mahitaji ya kupata huduma, muda wa kupata huduma na gharama kama zipo.

 

“Kwa lugha nyingine, Daftari hili limelenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika Utumishi wa Umma na kutoa fursa kwa wananchi wa ngazi zote kuongea na Serikali yao,” amesisitiza Bwana Kiwango

 

Bw. Kiwango amesema, Mfumo wa Daftari hilo upo tayari kwa kiwango kikubwa takriban 97%. “Ninaipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kusanifu na kujenga Mfumo huu wa Daftari la Huduma za Serikali kwa weledi na umahiri mkubwa, “ ameongeza.

 

Aidha, amewapongeza Waratibu wa mafunzo hayo ambao ni Idara ya Uendelezaji Taasisi chini ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kuona umuhimu wa kuwa na Timu ya wawezeshaji wa ndani watakaosambaza ujuzi huu kwa Taasisi nyingine.

 

Amesema Ofisi imeamua kuwajengea uwezo wa kuziwezesha Taasisi ili wawe na uelewa wa pamoja utakaopelekea kuwa na  Daftari litakalokidhi viwango. “Uelewa wenu wa kina utafanya Daftari kutekelezwa vema na Taasisi na kuwa na manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla,” amesisitiza.

 

Bw. Kiwango ametoa maelekezo mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Serikali Mtandao e-GA kutatua mapema iwezekanavyo changamoto za kimfumo za Daftari hilo zilizobainishwa wakati wa majaribio ya awali ili kutoa fursa kwa washiriki pindi mafunzo hayo yatakapokamilika iweze kuendelea kuziwezesha Taasisi za Serikali kuandaa Daftari hili, Waratibu wa mafunzo haya kupitia Idara ya Uendelezaji Taasisi, kuandaa mpango kazi utakaotumika kutekeleza jukumu hili kwa haraka.

 

Waratibu wa mafunzo na Wasimamizi wa mfumo kusimamia na kuhakikisha wawezeshaji hawabadiliki badiliki ili kupata tija ya mafunzo haya na Wawezeshaji wa GSD katika Taasisi za Serikali kuyachukulia  mafunzo haya kwa uzito mkubwa pindi wanapomaliza kwa kuwa wataenda kuwa walimu wa wengine katika Taasisi za Serikali.

 

 


 

Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini Bw. Priscus Kiwango  kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora akizungumza na Wawezeshaji wa Daftari la Huduma la Serikali  (GSD) kutoka kwenye  Taasisi za serikali wakati akifungua mafunzo ya siku tano  yanayofanyika  Mkoani Morogoro

 

Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini Bw. Priscus Kiwango  kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora akiwa na baadhi ya Wakurugenzi wakati  akifuatilia mafunzo ya  Daftari la Huduma la Serikali  (GSD)mara baada  kufungua mafunzo ya siku tano  yanayofanyika  Mkoani Morogoro

Mkurugenzi wa Idara ya uendeshaji Taasisi, Bw. Nolasco Kipanda kutoka Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora akitoa mafunzo kwa Wawezeshaji  wa Daftari la Huduma za Serikali kutoka kwenye Taasisi za Setikali  yanayofanyika kwa muda wa siku tano Mkoani Morogoro
Afisa Mchambuzi Kazi Bw. Macdonald kutoka Ofisi ya Rais,  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora akifundisha Wawezeshaji kutoka kwenye Taasisi za Serikali  kuhusu matumizi ya mfumo wa Daftari la Huduma za Serikali   jinsi ya kutumia mfumo wa daftari hilo katika mafunzo ya siku tano yanayofanyika Mkoani Morogoro.

Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini Bw. Priscus Kiwango kutoka Ofisi ta Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya  Wawezeshaji wa Daftari la Huduma la Serikali  (GSD) kutoka kwenye  Taasisi za Serikali wakati akifungua mafunzo ya siku tano  yanayofanyika  Mkoani Morogoro

 


 Afisa Uchumi Mwandamizi Nyang'anyi Chacha Gabriel kutoka Ofisi ya Rais - UTUMISHI na Utawala Bora  akiuliza baadhi ya  maswali kuhusiana na  matumizi ya nfumo wa Daftari la Huduma la Serikali (GSD)

na kupendekeza maboresho katika daftari hilo.

 

 

 


 

 

 



 


No comments:

Post a Comment