Na Mwandishi wetu-Dodoma.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi amezisisitiza Taasisi za Umma zilizoalikwa kushiriki Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kushiriki kikamilifu maonesho hayo yatakayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni, 2025 ili wananchi waweze kupata huduma za papo kwa hapo zitakazotolewa na Taasisi hizo huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo.
Katibu Mkuu Mkomi ametoa
msisitizo huo leo Jumatano, Mei 28, 2025 jijini Dodoma wakati wa Mkutano wake
na Waandishi wa Wahabari kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma
kitaifa.
Katibu Mkuu Mkomi amezitaja
huduma zitakazotolewa papo kwa hapo kuwa ni vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho
vya taifa (NIDA), hati za viwanja, kupima afya kutoka Hospitali za Benjamin
Mkapa, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Muhimbili, Taasisi ya Mifupa
(MOI) pamoja, huduma ya Gazeti la Serikali na nyingine nyingi.
“Nipende kutumia fursa hii
kuwakaribisha wakazi wa Jiji la Dodoma na maeneo jirani, Watumishi wa Umma na
wadau wa utumishi wa umma nchini kuhudhuria maonesho haya adhimu ili kujipatia
huduma hizo” amesema Bw. Mkomi.
Amesema katika maadhimisho hayo,
Wizara, Sekretarieti za Mikoa na Taasisi za Umma zitafanya maonesho hayo na
kutoa elimu kuhusu utekelezaji wa majukumu yao huku Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala
Bora itaendesha kliniki ya kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma
nchini papo kwa hapo.
Huduma
hizo za papo kwa hapo zinaenda sambamba na kaulimbiu ya maadhimisho hayo kitaifa
isemayo ‘‘Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijiti ili Kuongeza Upatikanaji wa
Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji’’
Akizungumzia umuhimu wa wananchi
kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo, Bw. Mkomi amesema Maadhimisho hayo
ya Wiki ya Utumishi wa umma ni jukwaa la Wananchi kupata fursa ya kufahamu
wajibu wao na haki zao ili pindi wanapokosa haki zao waweze kujua namna ya
kuzipata.
Vilevile, Bw. Mkomi ametaja faida
na malengo ya maadhimisho hayo kwa Taasisi za Umma kuwa zitapata fursa ya
kubadilishana uzoefu juu ya mbinu na mikakati mipya ya namna ya kutoa huduma bora
kwa Umma pamoja na kupokea ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo
Wananchi, AZAKI, na Sekta Binafsi juu ya namna bora ya kuboresha utoaji huduma.
Ameongeza kuwa, Taasisi hizo
zitapata fursa ya kuonyesha ubunifu waliofanya katika maeneo mbalimbali ya
utoaji huduma na kuondoa urasimu usiokuwa wa lazima katika michakato mbalimbali
ya utoaji huduma ikiwa ni pamoja na kupata mrejesho na kuutumia mrejesho huo
kurekebisha kasoro za utendaji zinazosababisha malalamiko ya wateja ili huduma
za Serikali ziboreshwe kukidhi matarajio ya Wananchi
Katika hatua nyingine Bw. Mkomi
amewataka Watumishi wa Umma wote,
kutimiza suala la kikatiba kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani Mwezi Oktoba, 2025 kujitokeza katika
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili muda wa uchaguzi utakapofika
waweze kuchagua viongozi bora kwa maendeleo ya taifa lao katika maeneo wanayofanyia
kazi.
Wiki ya Utumishi wa Umma nchini huanza tarehe 16 Juni kila mwaka na
huadhimishwa kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo maonesho, kutoa elimu na
huduma za papo kwa hapo ili kuifikia Siku ya Utumishi wa Umma ambayo
husherehekewa na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) tarehe 23 Juni kila
mwaka.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi akizungumza wakati Mkutano wake na Waandishi wa Wahabari kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kitaifa yatakayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni, 2025
No comments:
Post a Comment