Na
Happiness Shayo – Mwanza
Tarehe 28
Septemba, 2019
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa jengo la Kituo
cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kilichopo eneo la Pasiansi jijini Mwanza.
Akizungumza
wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa kituo hicho, Dkt. Mwanjelwa
amesema ujenzi wa mradi huo uko katika hatua nzuri hivyo, ameipongeza Idara ya
Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kwa kufikia hatua hiyo.
“Hakika jengo hili ni la viwango,
linaridhisha na vifaa vya ujenzi vilivyotumika viko katika viwango bora” Mhe.
Dkt. Mwanjelwa amefafanua.
Aidha,
Dkt. Mwanjelwa ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutenga bajeti
iliyowezesha ujenzi wa kituo hicho kwani mradi huo ulianza tangu mwaka 2008.
“Matumizi
ya mkandarasi na mshauri binafsi yalisababisha kuwapo kwa gharama kubwa za
ujenzi zilizosababisha kusimama kwa ujenzi katika hatua za awali, lakini mwaka
2017/2018 Serikali ya Awamu ya Tano ilithamini mradi na kutoa fedha zilizofanikisha
mradi kama unavyoonekana sasa” Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Kwa upande
wake, Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin
Msiangi amesema, Serikali iliamua kujenga kituo hicho cha Kumbukumbu na Nyaraka
za Taifa kwa lengo la kuhifadhi
kumbukumbu na nyaraka mbalimbali za ofisi za serikali zilizopo kanda ya ziwa.
Bw.
Msiangi amesema, kituo kitakapokamilika kitatumika kama kituo mbadala cha
kuhifadhi mifumo ya kumbukumbu na nyaraka iliyopo katika Kituo cha Taifa cha
Kumbukumbu cha jijini Dodoma.
Naye,
Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania, Mkoa wa Mwanza, Bw. Victor Baltazar
amemthibitishia Dkt. Mwanjelwa kuwa, ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa
kukamilika mwezi Novemba, 2019.
“Mpaka
sasa tumejenga jengo la utawala, maghala ya kuhifadhia nyaraka kwa asilimia 95
na pia tumejenga uzio, eneo la kuegesha magari, eneo la bustani, banda la
walinzi na madereva kwa asilimia 60” Bw. Baltazar amefafanua.
Ziara ya
Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa ya kutembelea kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa
jijini Mwanza ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake la kukagua utekelezaji
wa miradi iliyo chini ya Ofisi yake ikiwa ni pamoja na kuhimiza uwajibikaji kwa
watumishi wa umma nchini.
Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa
(Mb) akizungumza na watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa Kituo cha
Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Ziwa jijini Mwanza leo.