Waumini wa dini ya kikristo nchini wamehimizwa kutoa mchango kwenye maeneo
mbalimbali hususan katika kujenga
makanisa, shule na hospitali ambazo zitatumika kutoa huduma za kijamii kwa
ajili ya maendeleo ya taifa.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb)
wakati wa ibada ya kuwawekea mikono Mashemasi na Makasisi wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya
Kondoa iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji Mwema, Wilayani Kondoa.
Mhe. Mkuchika amewataka waumini wa kanisa hilo kuchangia maendeleo ya
kanisa, kwani mafundisho ya kanisa yanawataka waumini kutoa kwa hiyari ili
kuisaidia Serikali kuboresha huduma za kijamii ambazo ndio chachu ya maendeleo
ya taifa.
“Kanisa linatufundisha ni heri kutoa
kuliko kupokea kwa kuwa tukitoa tunapata thawabu kwa Mungu” Mhe. Mkuchika
amesisitiza.
Mhe. Mkuchika ameweka bayana kuwa, Kanisa la Anglikana Tanzania ni Kanisa
la tatu kuwa na wafuasi wengi lakini katika shughuli za maendeleo limekuwa
nyuma sana.
“Kanisa letu limekuwa nyuma katika uchangiaji wa shughuli za maendeleo hususan
kujenga makanisa mengine, shule na hospitali. Ni lazima tubadilike kwa sababu
Wamissionari wa Kigeni tuliowategemea sasa hawapo” Mhe. Mkuchika amesema.
Aidha, Mhe. Mkuchika alihamasisha uchangiaji wa ujenzi wa Kanisa ambapo
takribani milioni nne zilipatikana.
Naye, Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dkt. Given Gaula amemshukuru Mhe.
Mkuchika kwa kujitoa katika kuhamasisha uchangiaji wa maendeleo ya kanisa na
kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuleta maendeleo katika Taifa.
“Pamoja na masuala ya kiimani na kiroho, Kanisa la Anglikana limejipanga
kutoa elimu katika jamii kwa kujenga shule ya sekondari na ufundi katika Wilaya
ya Chemba na shule ya awali katika eneo la Bicha” Dkt. Gaula amesema na kuongeza
kuwa, kanisa hilo lina miradi mingine kama mradi wa hosteli na vikundi vya kijamii
vya kujikwamua kiuchumi vinavyojulikana kama Church Community
Mobilization Process.
Ibada ya kuwawekea mikono Mashemasi
na Makasisi imehudhuriwa na viongozi wa serikali wa wilaya ya Kondoa, washirika
wa Kanisa Anglikana kutoka Marekani, Uingereza na vikundi mbalimbali vya dini
kutoka kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) akizungumza wakati wa ibada
ya kuwawekea mikono Mashemasi na Makasisi wa Kanisa la Anglikana Tanzania,
Dayosisi ya Kondoa iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji Mwema, Wilayani
Kondoa.
Baadhi ya Mashemasi na Makasisi wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi
ya Kondoa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) (hayupo
pichani) wakati wa ibada ya kuwawekea mikono iliyofanyika katika kanisa la
Mchungaji Mwema, Wilayani Kondoa.
Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Rochester, Uingereza, James
Langstaff na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kondoa, Dkt. Given
Gaula, wakiwawekea mikono Mashemasi wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi
ya Kondoa wakati wa ibada iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji Mwema,
Wilayani Kondoa.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kondoa, Dkt. Given Gaula akizungumza
wakati wa ibada ya kuwawekea mikono Mashemashi na Makasisi wa Kanisa la
Anglikana Tanzania Dayosisi ya Kondoa iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji
Mwema, Wilayani Kondoa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) akiteta jambo na Mkuu wa
Wilaya ya Chemba, Mhe. Simon Odunga kabla ya kuanza kwa wa ibada ya kuwawekea mikono Mashemasi na
Makasisi wa Kanisa la Anglikana
Tanzania, Dayosisi ya Kondoa iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji Mwema,
Wilayani Kondoa.