Thursday, September 15, 2016

USIMAMIZI WA MAADILI KWA VIONGOZI WA UMMA


Makala iliyopita Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora  Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) aliongea kuhusu hatua zinazochukuliwa kuondoa Watumishi wasiostahili kuwepo katika orodha ya malipo ya Serikali (payroll). Aidha, alieleza hatua zinazochukuliwa kwa wote waliobainika kusababisha malipo yasiyostahili. Waziri Kairuki aliongea hayo katika Runinga ya Taifa (TBC), makala ya leo inaangalia suala la Maadili kwa viongozi wa Umma, Nyaraka za Serikali na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Serikalini.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akitoa maelekezo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Said wakati wa kikao kuhusu masuala ya kiutumishi na viongozi wa mkoa wa Tanga. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigela.

Usimamizi wa Maadili kwa viongozi wa Umma ukoje?

Waziri Kairuki alieleza kumekuwepo na malalamiko ya ukiukwaji wa maadili dhidi ya viongozi wa Umma na hadi kufikia Agosti 2016, malalamiko 200 yalipokelewa ambapo kati ya malalamiko hayo, malalamiko 142 yalihusu Sheria ya Maadili na malalamiko 58 hayakuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

“Uchunguzi wa awali umefanyika kwa malalamiko 11 yanayohusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili. Aidha, malalamiko 58 ambayo hayakuhusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma walalamikaji walipewa ushauri na mengine yalielekezwa kwenye mamlaka zinazohusika. Malalamiko hayo yalihusu pamoja na mambo mengine masuala ya rushwa na migogoro ya ardhi” Mhe. Kairuki alifafanua katika kipindi cha TBC. 

Aliongeza, hatua zinazochukuliwa dhidi ya Viongozi wa Umma wanaothibitika kukiuka Sheria ya Maadili ni pamoja na kufikishwa katika Baraza la Maadili lililoundwa kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kufanya uchunguzi wa kina.

Kuanzia mwaka 2010/11 hadi 2015/16 jumla ya mashauri 69 ya ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma yalifanyiwa kazi na Baraza la Maadili, kati yake mashauri 38 yalithibitika kukiuka Sheria ya Maadili na Viongozi na wahusika kupewa adhabu mbalimbali ikijumuisha Onyo (12), Onyo Kali (19), Faini ya shilingi milioni moja (1), kushushwa cheo (3) na kuondolewa katika wadhifa (3).

Waziri Kairuki mwenye dhamana na Utumishi wa Umma na Utawala Bora nchini alisema miongoni mwa mashauri hayo yalihusu kutowasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni, kutoa tamko la uongo, matumizi mabaya ya madaraka na mali ya Umma na mpaka wakati huu  Sekretarieti ya Maadili ina malalamiko 12 yakufikisha mbele ya Baraza la Maadili.

Pamoja na hayo, alisema ipo mikakati ambayo Serikali inaitumia katika kukuza maadili ya viongozi wa umma nchini ikiwamo kutoa elimu kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambapo katika mwaka wa fedha 2015/16, Viongozi wa Umma 7,442 walipatiwa elimu kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mgongano wa Maslahi na Maadili ya Utumishi wa Umma.

Hali ikoje kuhusu Nyaraka na Siri za Serikali?
“ Kwa mujibu wa Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1970 na Sheria ya Kumbukumbu na Nyaraka ya Mwaka 2002 ni kosa la Jinai kwa mtu yeyote kutoa au kuvujisha taarifa zenye zuio kwa wasio walengwa”  Waziri Kairuki alisema.

Aliainisha kuwa Serikali  imekuwa ikichukua hatua kuhusu hilo ikiwamo kuwashitaki wahusika mahakamani kwa kuvunja sheria, Kuwachukulia hatua za kinidhamu Watumishi wa Umma na hatimaye kufukuzwa kazi, kushushwa cheo na kupunguziwa mshahara.

Aliongeza mengine yanayofanyika ni pamoja na kutoa elimu kwa Watumishi na wananchi juu ya Sheria na Kanuni zinazosimamia masuala ya utoaji wa taarifa, nyaraka na siri za Serikali.  

Mhe. Kairuki alisema hatua nyingine zinazochukuliwa ni kuendelea kusimamia Sheria ya Usalama wa Taifa Na. 3 ya mwaka 1970 na Sheria ya Kumbukumbu na Nyaraka ya Mwaka 2002, Mwongozo wa Matumizi Bora, Sahihi na Salama ya Vifaa vya TEHAMA wa mwaka 2012 na Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma za mwaka 2005, pia kuimarisha matumizi na usalama wa mifumo ya TEHAMA ili kudhibiti uvujaji wa nyaraka na siri za Serikali kupitia mitandao ya kijamii.

Matumizi ya TEHAMA yakoje Serikalini?
Waziri Kairuki alisema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yamepunguza gharama za uendeshaji wa kazi mbalimbali za Serikali akitolea mfano wa uendeshaji wa semina na mikutano kwa njia ya mawasiliano ya video (Video Conference) ambapo mikutano ya Serikali hufanyika kwa gharama nafuu kwani haimlazimu mshiriki kusafiri; na uendeshaji wa mafunzo ambapo mwezeshaji mmoja anaweza kuendesha mafunzo kwa watendaji katika zaidi ya kituo kimoja.

Alisema hadi sasa huduma hiyo ipo katika Mikoa yote isipokuwa mikoa ya Geita, Katavi, Njombe, Simiyu na Songwe ambayo Serikali ipo katika mkakati wa kufikisha huduma hiyo, pamoja na hilo taasisi 77 zimeunganishwa kwenye Mtandao wa Mawasiliano ya Serikali (GovNet) hivyo kufanya mawasiliano kulipia muda wa maongezi.

“Azma ya Serikali  ni kutatua kero  zinazowakabili wananchi katika kupata huduma mbalimbali katika Taasisi za Umma” Waziri Kairuki alisema na kuelezea utekelezaji wa miradi kama Mawasiliano ya ndani ya ofisi (electronic Office) kupitia Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Wakala ya Serikali Mtandao (eGA), Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka (electronic Records) kupitia Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Ununuzi wa Umma kwa njia ya Mtandao (e-Procurement system) kupitia PPRA na MSD, na Huduma za Kitabibu kwa njia ya mtandao (Telemedicine system) kupitia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.




***Itaendelea - Sehemu ijayo itahusu suala la mapambano ya  rushwa na mpango wa uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi.

1 comment:

  1. Ahsante Mheshimiwa nashukuru kwa kutoa ufafanunuzi wa kina juu ya maadili ya viongozi wa umma, Napenda kuwaomba endeleeni kutoa Elimu kwa wahusika,
    Maana Heshima na Nidhamu ni mafanikio mema ya kazi

    ReplyDelete