Friday, March 19, 2021
Thursday, March 18, 2021
Monday, March 15, 2021
TASAF KUJENGA WODI YA AKINA MAMA NA MAABARA KIJIJI CHA MKAMBARANI
Na. James K. Mwanamyoto-Morogoro
Tarehe 15 Machi, 2021
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameiahidi Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kupitia TASAF kujenga wodi ya
kuwahudumia akina mama wajawazito na maabara katika zahanati ya Kijiji cha Mkambarani
ili wananchi wa kijiji hicho wapate huduma bora za afya.
Mhe. Ndejembi ametoa ahadi hiyo ikiwa ni utekelezaji
wa maelekezo ya kamati hiyo ya kudumu iliyoelekeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF) kujenga jengo la kina mama kwa ajili ya kuwapatia huduma stahiki, ikiwa
ni pamoja na kujenga maabara itakayotoa huduma bora ya vipimo kwa wananchi wa Kijiji
cha Mkambarani.
Mhe. Ndejembi amesema, kutokana na maelekezo
yaliyotolewa na kamati ofisi yake itajenga wodi ya akina mama ili kuwe na
faragha wakati wa kuwahudumia akina mama wajawazito.
Kuhusu maelekezo ya ujenzi wa maabara, Mhe. Ndejembi
ameihakikishia kamati na wananchi wa Kijiji cha Mkambarani kujenga maabara ili
kuwaondolea adha wananchi hao ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya
maabara ambapo pia hulazimika kuingia gharama kubwa.
Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, lengo la
Serikali kujenga zahanati ya Mkambarani ni kuwasogezea karibu huduma za afya
wananchi wa eneo hilo ikizingatiwa kuwa, walengwa wa TASAF watanufaika pia na
huduma zinazotolewa na zahanati hiyo na hatimaye kuwa na afya bora
itakayowawezesha kupambana na umaskini kupitia ruzuku ya TASAF wanayoipata.
Awali, akitoa maelekezo kwa Serikali kwa niaba
ya kamati yake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali
za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) amesema Kamati imelazimika kutoa
maelekezo ya ujenzi wa Wodi ya akina mama na maabara kama sehemu ya kulinda utu
wa wananchi hususani akina mama wanaofuata huduma ya uzazi katika zahanati ya
Mkambarani.
Mhe. Polepole amesema, wodi ya akina mama
ikijengwa itaongeza usiri na faragha wakati wa kuwahudumia wajawazito tofauti
la ilivyo sasa ambapo hakuna usiri wa kutosha wala faragha pindi akina mama
wanapohudumiwa.
Kuhusiana na maelekezo ya ujenzi wa maabara,
Mhe. Polepole ameeleza kuwa, kamati yake imepata fursa ya kuitembelea zahanati
ya Mkambarani na kubaini kuwa hakuna maabara inayokidhi mahitaji ndio maana
kamati yake imeielekeza Serikali kujenga maabara itakayokidhi kutoa huduma
stahiki kwa wananchi wa Kijiji cha Mkambarani.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na
Serikali za Mitaa imemaliza ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Dar es Salaam, Pwani
na Morogoro iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na taasisi
zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali
za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) akitoa maelekezo kwa Serikali kuhusu
ujenzi wa wodi ya kuwahudumia akina mama wajawazito na maabara katika zahanati
ya Kijiji cha Mkambarani.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mkambarani-Morogoro wakimsikiliza
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe.
Humphrey Polepole (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo
iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF kijijini hapo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali
za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) na baadhi ya wajumbe wa kamati yake
pamoja na watendaji wa Serikali wakikagua zahanati ya Mkambarani wakati wa
ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya
TASAF kijijini hapo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza kuhusu utekelezaji wa
maelekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati
wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya
TASAF katika Kijiji cha Mkambarani - Morogoro.
Mmoja wa wanufaika wa TASAF wa Kijiji cha Mkambarani Mzee
Abdallah J. Kinyaku akitoa ushuhuda wa namna alivyonufaika na TASAF kwa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa ziara ya kikazi ya
kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa mpiradi ya TASAF kijijini hapo.
TASAF KUBORESHA BWAWA LA MAJI KIJIJI CHA KALOLENI ILI KUWAPATIA WANANCHI MAJI SAFI NA SALAMA
Na. James K. Mwanamyoto-Chalinze
Tarehe 14 Machi, 2021
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameiahidi Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuboresha mfumo wa bwawa la
maji Kijiji cha Kaloleni kata ya Ubena Zomozi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya
Chalinze ili kuwapatia wananchi wa eneo hilo maji safi na salama.
Mhe. Ndejembi ametoa ahadi hiyo ikiwa ni
sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya kamati iliyoitaka Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF) kurekebisha mfumo wa bwawa hilo ili kuwapatia maji safi na salama
wananchi wa kaloleni na vijiji jirani.
Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, licha ya mradi
wa bwawa hilo kujengwa wakati wa awamu ya kwanza ya utekelezaji wa TASAF lakini
kutokana na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama inayowakabili
wananchi wa eneo la Kaloleni na vijiji jirani, Serikali itafanya marekebisho
kuwawezesha wananchi kupata huduma hiyo ya maji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF
Bw. Ladislaus Mwamanga amesema, ofisi yake itapeleka wataalam mapema
iwezekanavyo ili kufanya tathmini ya namna bora ya kuboresha bwawa hilo.
Bw. Mwamanga ameongeza kuwa, fedha ya kufanya
maboresho hayo ipo kwani mradi huo ni kipambule cha Serikali katika Utekelezaji
wa Mradi wa kipindi cha pili cha Awamu ya Tatu kilichozinduliwa hivi karibuni
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Awali akitoa maelekezo juu ya uboreshaji wa
bwawa hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za
Mitaa Mhe. Humphrey Polepole (Mb) amesema, kamati imelazimika kutoa maelekezo
hayo kutokana na umuhimu wa bwawa hilo
kwa wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani.
Aidha, Mhe. Polepole amewataka wasimamizi wa
mradi na wananchi kuhakikisha wanalitunza bwawa hilo ili wanufaike na uwepo
wake kama Serikali ilivyokusudia.
Mradi wa bwawa la maji Kaloleni ulijengwa katika kipindi cha kwanza cha utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Awamu ya Kwanza kwa lengo la kuwapatia maji safi na salama wananchi wa Kaloleni na vijiji jirani, ikiwa ni pamoja na kuiwezesha mifugo yao kupata maji ya kunywa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) akitoa maelekezo ya kuboresha
mfumo wa bwawa la maji la Kijiji cha Kaloleni kata ya Ubena Zomozi kwa niaba ya
kamati anayoiongoza.
Baadhi ya wananchi wa Kaloleni kata ya Ubena
Zomozi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze wakisikiliza Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey
Polepole (Hayupo pichani) wakati akitoa maelekezo ya kuboresha mfumo wa bwawa
la maji la kijiji chao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) akikagua mradi wa
bwawa la maji la Kijiji cha Kaloleni kata ya Ubena Zomozi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) akiteta jambo na Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi mara baada ya kukagua mradi wa bwawa la maji la Kijiji cha
Kaloleni kata ya Ubena Zomozi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiiahidi Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuboresha mfumo wa bwawa la maji
Kijiji cha Kaloleni kata ya Ubena Zomozi ili kuwapatia wananchi wa eneo hilo
maji safi na salama.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus
Mwamanga akiiahidi Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuleta
wataalam kufanya tathmini ya namna bora ya kuboresha bwawa la Kijiji cha
Kaloleni kata ya Ubena Zomozi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) akiwa katika picha ya
pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati yake na watendaji wa Serikali mbele ya mradi
wa bwawa la maji la Kijiji cha Kaloleni kata ya Ubena Zomozi.
Saturday, March 13, 2021
CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA CHATAKIWA KUENDELEA KUJENGA NIDHAMU NA UADILIFU KWA WATUMISHI WA UMMA
Na.
James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam
Tarehe 13 Machi, 2021
Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Humprey Polepole (Mb)
amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kina jukumu la kuhakikisha kinaendelea
kujenga nidhamu na uadilifu kwa watumishi wa umma na viongozi katika Utumishi
wa Umma ili waweze kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.
Mhe. Polepole ametoa rai hiyo mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa anayoiongoza kutembelea makao makuu ya Chuo cha Utumishi wa Umma jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya chuo hicho chenye dhamana ya kutoa mafunzo kwa Watumishi wa Umma yanayowawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mhe. Polepole amesema, chuo hakina budi kuendelea kutoa mafunzo yenye tija ili kizazi kipya kilichoingia na kinachoendelea kuingia katika Utumishi wa Umma kiendelee kuishi katika mila, utamaduni, desturi na miiko ya Utumishi wa Umma.
Mhe. Polepole amefafanua kuwa, Utumishi wa Umma nchini umejengeka katika mila, utamaduni, na desturi, hivyo Chuo cha Utumishi wa Umma pekee ndio kina jukumu la msingi kuhakikisha kinatoa mafunzo ambayo yatajenga utamaduni utakaoimarisha nidhamu ya utendaji kazi, uadilifu na uzalendo kwa Watumishi wa Umma.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na
Serikali za Mitaa kuwa, suala la kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma kiutendaji
na nidhamu limepewa uzito unaostahili na ofisi yake kwa kuwataka waajiri wote
kuhakikisha wanatenga bajeti itakayowawezesha watumishi wao kupata mafunzo
yanayotolewa katika Chuo cha Utumishi wa Umma.
Aidha, Mhe. Ndejembi amewaomba wajumbe wa kamati hiyo kutumia mamlaka waliyonayo kushirikiana na Ofisi yake kuwahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Taasisi za Umma kutenga fedha zitakazowawezesha Watumishi wa Umma kupata mafunzo katika Chuo cha Utumishi wa Umma.
Mhe. Ndejembi ameiahidi kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ili kuboresha huduma zinazotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.
Chuo
cha Utumishi wa Umma Tanzania kilianzishwa kwa lengo la kutoa mafunzo katika
Nyanja za uongozi, menejimenti na utawala kwa ngazi za Cheti, Stashada na
Astashahada. Pia chuo kinafanya utafiti na kutoa ushauri wa kitaalam.
Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humprey Polepole (Mb) akiwahimiza
Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Kampasi ya Dar es Salaam
kutoa mafunzo yatakayowajengea Watumishi wa Umma nchini nidhamu ya Utendaji
kazi na uadilifu.
Baadhi
ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa na
watumishi wa TPSC wakisikiliza maelekezo ya Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe.
Humprey Polepole (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo yenye lengo la
kukagua utekelezaji wa majukumu ya TPSC.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza
na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (hawapo
pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo katika Chuo cha Utumishi wa
Umma yenye lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya chuo hicho.
Baadhi
ya watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Dar es Salaam
wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za
Mitaa, Mhe. Humprey Polepole (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo
yenye lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya TPSC.
Mjumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Saashisha
Mafue ambaye ni mnufaika wa mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma
akitoa ushuhuda wa namna alivyopata mafunzo katika chuo hicho wakati wa ziara
ya kikazi ya kamati hiyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya
TPSC.
Mtendaji
Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Dkt. Emmanuel Shindika
akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya chuo chake kwa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo
yenye lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya TPSC.
Monday, March 8, 2021
WATUMISHI WANAWAKE NI WACHAPAKAZI MAHIRI KATIKA UTUMISHI WA UMMA
Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe
08 Machi, 2021
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael amesema Watumishi wa Umma wanawake ni wachapakazi mahiri katika Utumishi wa Umma nchini.
Dkt.
Michael amepongeza uchapakazi wa watumishi wanawake mapema leo wakati akitoa
ujumbe maalum wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Wanawake
duniani Machi 8, 2021 ikiwa ni sehemu ya ofisi yake kutambua mchango wa
Watumishi wa Umma wanawake katika utoaji huduma kwa wananchi.
Ameongeza kuwa, kwa upande wa Wakurugenzi Wasaidizi ofisi ina jumla ya Wakurugenzi Wasaidizi 22, kati ya hao 12 ni wanawake ambao ni sawa na asilimia hamsini na tano (55%) wakati 10 ni wanaume ambao ni sawa na asilimia arobaini na tano (45%).
“Ukitazama takwimu ya idadi ya Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi waliopo katika Ofisi yetu inadhihirisha kuwa, Ofisi imetoa fursa za uongozi kwa wanawake ambao pasipo na shaka yoyote wameuthibitishia umma kuwa, wana uwezo kiutendaji kwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu”, amefafanua Dkt. Michael.
Dkt. Michael ametoa wito kwa waajiri katika Taasisi za Umma kuhakikisha wanawashirikisha watumishi wanawake katika masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya taasisi zao kwani wanao uwezo kiutendaji katika kuhakikisha taifa linapata maendeleo.
Aidha, ametoa wito kwa Watumishi wa Umma katika Taasisi zote za Umma kuwapa ushirikiano wa dhati viongozi wanawake walioteuliwa na mamlaka mbalimbali ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Sanjali na hilo, amewataka Watendaji Wakuu katika Taasisi za Umma kuwapendekeza wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi ili kutoa fursa kwa wanawake kushiriki katika ujenzi wa taifa.
Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kama msimamizi wa
masuala ya kiutumishi na utawala bora nchini inaungana na Watanzania na wadau
wote Kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2021, ikiwa ni sehemu ya
kutambua mchango wa viongozi wanawake katika Utumishi wa Umma kama kaulimbiu ya
maadhimisho ya mwaka huu inavyojianisha kuwa “Wanawake katika Uongozi: Chachu kufikia Dunia yenye Usawa”.
Kaimu Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael akitoa
ujumbe kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2021, ikiwa ni sehemu
ya kutambua mchango wa Watumishi wa Umma wanawake katika kutoa huduma kwa
wananchi.
Afisa
Habari wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi.
Veronica Mwafisi akifanya mahojiano na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael kuhusu Maadhimisho ya Siku ya
Wanawake Duniani Machi 8, 2021.
Baadhi
ya Watumishi wa Umma wanawake wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kushiriki Maadhimisho ya
Siku ya Wanawake kimkoa Machi 8, 2021 jijini Dodoma.
Baadhi
ya Watumishi wa Umma wanawake wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora wakiwa katika maandamano ya Siku ya Wanawake kimkoa Machi 8,
2021 jijini Dodoma.