|
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Rais-Utumishi Bw.Florence Temba (wa pili kutoka kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mawasiliano kwa njia ya video serikalini (video conferencing)katika mkutano uliofanyika Idara ya HABARI (MAELEZO) leo.Wengine ni viongozi wa Ofisi ya Rais-Utumishi.Wengine ni Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) Bw.Charles Senkondo (wa pili kutoka kushoto),Mkurugenzi wa TEHAMA Bw.Priscus Kiwango (kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi ,Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Bw.Peter Mushi (kulia). |
|
Maafisa wa Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Idara ya HABARI (MAELEZO) leo. |
|
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) Bw.Charles Senkondo (wa pili kutoka kushoto) akitoa ufafanuzi kuhusu mawasiliano kwa njia ya video serikalini (video conferencing)katika mkutano uliofanyika Idara ya HABARI (MAELEZO) leo.Wengine ni Mkurugenzi wa TEHAMA Bw.Priscus Kiwango (kushoto), Mkurugenzi Msaidizi ,Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Bw.Peter Mushi (kulia) na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Rais-Utumishi Bw.Florence Temba (wa pili kutoka kulia). |
|
Mkurugenzi wa TEHAMA Ofisi ya Rais-Utumishi Bw.Priscus Kiwango (kushoto)akifafanua namna mikutano kwa njia ya video serikalini inavyofanyika katika kikao na waandishi wa habari kilichofanyika Idara ya HABARI (MAELEZO) leo.Wengine ni Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) Bw.Charles Senkondo (katikati) na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bw.Florence Temba ( kulia). |
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS
Simu ya Upepo "UTUMISHI",
DSM. Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma,
Simu: 2118531/4 au 2122908 Utumishi
House,
Fax: 2125299 8 Barabara ya Kivukoni,
11404 Dar es Salaam,
Unapojibu tafadhali taja:
MIKUTANO
KWA NJIA YA VIDEO SERIKALINI
Maendeleo ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yamebadilisha namna ya uendeshaji
wa shughuli za Serikali kiasi cha kuilazimu kuchukua hatua madhubuti ili kuendana na mabadiliko hayo. Moja kati ya
hatua hizo ni kuendesha mikutano kwa njia ya Video.
Mawasiliano kwa njia
ya video (Video Conferencing) ni teknolojia inayowawezesha wahusika walioko vituo/sehemu
mbalimbali kuwasiliana kwa njia ya sauti na picha hivyo kuwezesha wahusika
kuonana na kusikilizana pasipo kukutana sehemu moja.
Teknolojia hii inasaidia
kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za mawasiliano kwa kuwa hailazimu wajumbe
kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine. Aidha, inawezesha mawasiliano
kufanyika kwa ufanisi, kupunguza muda wa kuhudhuria mikutano, kuweka kumbukumbu
sahihi za mikutano na kuongeza tija katika utendaji kazi Serikalini.
Ili kuwezesha kuwepo kwa mawasiliano hayo kati
ya kituo kimoja na kingine ni lazima kuwepo kwa rasilimali muhimu kama vile miundombinu
ya mawasiliano pamoja na vifaa mbali
mbali vya TEHAMA katika vituo hivyo. Katika jitihada za kuziwezesha Taasisi za Umma kushirikiana
katika matumizi ya rasilimali za TEHAMA ili kuondoa urudufu, kupunguza gharama
na kuongeza ubora wa huduma kwa umma, Serikali
imejenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB).
Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano umejengwa hadi katika makao makuu ya baadhi ya Wilaya na Mikoa yote ya Tanzania bara. Hatua hii imeweka msingi
imara wa mawasiliano ya kielektoniki. Sambamba na hilo, Serikali imesambaza
vifaa vinvyotumika kwa mawasiliano ya video katika Mikoa yote isipokua Geita, Katavi, Njombe na Simiyu ambayo ni
mipya.
Hivi
sasa, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya wa Umma Utumishi (OR-MUU) inaendelea kujenga Mtandao
wa Serikali wa Mawasiliano (GovNet)
ambao unatumia kwa kiasi kikubwa miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano. Lengo kubwa la mtandao wa GovNet ni kuziwezesha Taasisi za
Serikali kuwa na mawasiliano ya kielektoniki (data, sauti na picha) ya ndani
yenye usalama na gharama nafuu. Mtandao unalenga kuunganisha jumla ya Taasisi
72 ambazo ni Wizara zote, Idara zinazojitegemea 16 na Wakala za Serikali 30.
Mtandao huo pia utaziunganisha Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Serikali
za Mitaa 77.
Mafanikio ya mtandao
huo yameanza kuonekana ambapo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma imechukua hatua ya kuendesha mikutano kazi kwa
njia ya Mawasiliano ya Video. Jambo hili linawawezesha watendaji serikalini kupata
muda zaidi wa kutoa huduma kwa wananchi na kusimamia utekelezaji wa kazi
mbalimbali.
Mkutano mmoja una
uwezo wa kuchukua idadi ya wajumbe zaidi ya 150 ambao hupata nafasi ya kuongea
(interactivity) kwa muda wanaopangiwa. Wastani wa muda wa mkutano ni saa 5. Hadi
kufika mwaka huu (2015), awamu kumi (10)
za mikutano kazi zimefanyika toka ilipoanza mwishoni wa mwaka 2013, zikihusisha
mikoa takribani yote.
Taratibu za
uendeshaji wa mikutano hii kwa kutumia Mawasiliano ya Video ni sawa na mikutano mingine ambapo huongozwa
na Mwenyekiti (Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma) na
wahusika hupewa ratiba ya matukio na mada mapema kabla ya siku ya mkutano
husika. Mkutano mmoja huweza kuunganisha
mikoa hadi kumi (10) kwa pamoja. Walengwa wakuu wa mikutano hiyo ni Makatibu
Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi, na Maafisa Utumishi wa Mamlaka za Serikali za
Mitaa pamoja na maafisa wengine watendaji katika taasisi hizo. Mikutano hii
imeweza kufanikishwa kwa kiasi kikubwa kutokana na ushirikiano mkubwa unaotoka
Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, Sekretarieti za Mikoa na TAMISEMI.
Mfumo wa kuendesha
mikutano serikalini kwa njia ya video ni salama kutokana na miundombinu yote inayotumika kuratibiwa na wataalamu
wa serikali. Hakuna matumizi ya mifumo ambayo ni wazi ambayo inaweza
kuhatarisha mawasiliano kunaswa na mtu asiyehusika. Katika maeneo ambayo
miundombinu ya TEHAMA haijatengamaa sawa sawa, watendaji hutumia ofisi zilizo jirani
na maeneo yao ya kazi ili kufanikisha mikutano kazi hiyo. Hata hivyo, Matarajio
ni kuwezesha ofisi za Serikali kuwa na vifa vya kisasa vya TEHAMA na
kuunganishwa kwenye miundombinu iliyopo ili kuongeza ufanisi na tija katika
kutoa huduma kwa wananchi
Katika kuhakisha
usimamizi na uendeshwaji bora wa mikutano hii, hivi sasa umeandaliwa mwongozo
wa kuendesha mikutano kwa njia ya video “Mwongozo wa Mawasiliano kwa Njia ya
Video Serikalini” na kila mwajiri katika Taasisi ya Serikali anawajibika kuutumia
ili kutekeleza jambo hili muhimu.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Kny:
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma